Taasisi 2 za kuteua wauguzi watakaohudumu Saudi Arabia zatambuliwa

Martin Mwanje
2 Min Read

Wizara ya Leba na Ulinzi wa Jamii imetambua mashirika mawili ya kibinafsi yanayoshughulika na masuala ya ajira nchini ili kusaidia katika uteuzi wa wauguzi watakaotumwa kuhudumu nchini Saudi Arabia.

Hususan, mashirika hayo yatasaidia katika uwianishaji wa ujuzi wa wauguzi hao na mahitaji ya Saudia.

Katibu katika Wizara ya Afya Mary Muthoni ametaja mashirika ya Fast Reliable Entreprises na NASMAMA Services Ltd kuwa yatakayosaidia katika uteuzi wa wauguzi 2,500 watakaotumwa kuhudumu nchini Saudia Arabia.

Muthoni amesema mashirika hayo mawili yalichaguliwa baada ya kufanyika kwa zoezi la utathmini wenye ushindani mkali.

Miongoni mwa nyaraka wanazohitaji kuwasilisha wakati wanapotuma maombi, wauguzi wanaotaka kuhudumu nchini Saudia wametakiwa kuwasilisha wasifu wao ukielezea umri, uzito na urefu wao, cheti halali cha baraza la uuguzi na cheti cha kudhirisha tajiriba yao ya utendakazi waliopata baada ya kupita mitihani ya vyeti.

“Maelezo haya ya kina yatahakikisha mchakato wa uteuzi unakidhi viwango vya utoaji huduma za afya na mahitaji ya Saudi Arabia, na kudhihirisha kujitolea kwetu kutoa wataalam wenye ujuzi wa hali ya juu,” alisema Katibu Muthoni katika taarifa.

Wauguzi wanaotaka kutuma maombi wametakiwa kuwasiliana moja kwa moja na mashirika yaliyoteuliwa ili kupashwa habari zaidi kuhusiana na mchakato wa utumaji maombi au kutembelea tovuti ya Shirika la Kitaifa la Ajira, NEA ambayo ni www.neaims.go.ke.

 

 

Share This Article