Baraza kuu la Waislamu nchini SUPKEM limeishukuru serikali kwa hatua yake ya kusambaza chakula kwa waisilamu wanaohitaji msaada huku wakianza kuadhimisha mwezi mtukufu wa Ramadhan.
Msemaji wa serikali Isaac Mwaura, alianzisha usambazaji huo Jumamosi katika kaunti ya Nairobi.
Mwenyekiti wa kitaifa wa SUPKEM Hassan Ole Naado, alitoa wito kwa waumini wa dini ya kiislamu kuzingatia umoja na kukumbatia ukarimu wakati huu wa mfungo.
Baraza hilo limewataka waumini hao pia kutogawanyika kuhusu kuanza kwa Ramadhan, maadhimisho ambayo huanza pindi mwezi unapoonekana.
Serikali inasambaza vyakula vya thamani ya shilingi milioni 124.5 kwa waisilamu wasiojimudu katika kaunti 19, vyakula watakavyotumia wakati wa Ramadhan.
Mpango huo unatekelezwa na idara ya serikali ya maeneo kame na maendeleo kwa lengo la kuwezesha waisilamu wasiojiweza kuadhimisha vyema mfungo wa Ramadhan.
Katibu katika idara hiyo, Kello Harsama, alielezea kwamba Rais William Ruto ndiye aliidhinisha usaidizi huo kwa waisilamu ili wapate vyakula faafu wakati huu muhimu wa dini yao bila kukwazwa na hali yao ya kiuchumi.
Kaunti zinazolengwa kwa usambazaji wa chakula hicho ni Marsabit, Garissa, Mandera, Wajir, Mombasa, Lamu, Nakuru, Baringo na Isiolo. Nyingine ni Mombasa, Kitui, Nyeri, Uasin Gishu, Kakamega, Machakos, Taita Taveta, Kwale, Kilifi na Nairobi.