Spika Wetang’ula asema Kenya iko tayari kuendeleza uhusiano mwema na Iran

Marion Bosire
1 Min Read

Spika wa bunge la taifa Moses Wetang’ula leo asubuhi alikuwa mwenyeji wa balozi wa taifa la Kiisilamu la Iran nchini Kenya Ali Gholampour, aliyemtembelea afisini mwake.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Facebook, Wetang’ula alielezea kwamba yeye na balozi Ali walizungumzia uhusiano wa muda mrefu ambao umekuwepo kati ya mataifa hayo mawili.

Uhusiano huo, kulingana naye, uliota hata kabla ya Kenya kujipatia uhuru kutoka kwa wakoloni na ukaendelea hadi ubalozi wa Iran nchini ulipoanzishwa wakati wa utawala wa Rais Moi.

Mazungumzo ya wawili hao yaligusia uwekezaji, kuimarisha biashara, kuimarisha uvumbuzi wa kiteknolojia, maendeleo ya miundombinu, na kukuza sera nzuri za mambo ya nje.

Walizungumza pia juu ya uwezo uliopo wa kuboresha hata zaidi mahusiano ya nchi za Kenya na Iran kupitia urafiki kati ya makundi mbalimbali ya bunge.

Kituo cha utafiti cha bunge la nchi ya Iran kinatoa fursa nyingi za ushirikiano katika nyanja kama vile kujenga uwezo, utafiti na usambazaji wa taarifa kati ya taasisi hizo mbili.

“Katika kutambua uthabiti na uwezo wa Iran, nilidhihirisha nia ya Kenya ya kuimarisha misingi ya heshima ya pande zote mbili na ushirikiano,” aliongeza Wetang’ula.

Share This Article