Spika wa bunge la taifa Moses Wetangula hivi leo alikuwa mwenyeji wa balozi wa Cyprus nchini Bwana Savvas Vladimirou, katika afisi yake kwenye majengo ya bunge.
Wetangula alimkaribisha Vladimirou nchini rasmi baada ya taifa la Cyprus kufungua tena ubalozi wake humu nchini.
Alisifia hatua ya serikali ya nchi hiyo akisema itaboresha uhusiano mwema kati ya Kenya na Cyprus.
“Kurejea kwa Cyprus nchini Kenya kunaashiria kilele cha uhusiano wa kihistoria ulioanza miaka ya 1950” Alisema Spika Wetangula.
Alikumbuka uhusiano uliokuwepo awali kati ya Rais wa kwanza wa Kenya Hayati Mzee Jomo Kenyatta, na Rais wa kwanza wa Cyprus askofu mkuu Makarios.
Kulingana naye Kenya ilikuwa makao salama kwa Rais Makarios wakati wa majaribio ya kupindia serikali na hilo liliboresha hata zaidi uhusiano kati ya nchi hizi mbili.
Wetangula alimtajia balozi Savvas Vladimirou kwamba wakenya mashuhuri kama aliyekuwa naibu rais Kalonzo Musyoka walipata elimu ya juu nchini Cyprus akisema kwamba nchi hiyo inatoa fursa nzuri
za elimu kwa wakenya.
Vladimirou kwa upande wake aliangazia hatua zilizochukuliwa na nchi yake ili kuboresha uhusiano na Kenya akisisitiza kwamba utakuwa wa maana sana kwa wananchi wa nchi zote mbili.
Wawili hao walizungumzia pia nyanja mbali mbali ambazo nchi hizi mbili zinaweza kushirikiana.