Spika Wetang’ula ahimiza wakulima kurejelea kilimo cha pamba

Marion Bosire
1 Min Read

Spika wa bunge la taifa Moses Wetang’ula amehimiza wakulima hasa wa kaunti ya Busia kurejelea kilimo cha pamba huku serikali ikipania kufufua viwanda vya kutayarisha pamba katika eneo hilo.

Wetang’ula alikuwa akizungumza katika kikao cha wazee wa jamii wa Marachi kufuatia mwaliko wa mbunge wa eneo la Butula Joseph Oyula.

Katika kikao hicho, wazee wa jamii ya Marachi waliwasilisha maombi yao kuhusu mambo mbalimbali ambayo wangependa yashughulikiwe na serikali kuu.

Wazee hao walipendekeza kuanzishwa kwa kituo cha utamaduni katika eneo hilo kwa lengo la kukuza na kuhifadhi utamaduni wa Marachi kwa ajili ya vizazi vijavyo.

Wanapania pia kuhakikisha ujenzi wa kituo cha utafiti, maendeleo na teknolojia cha Butula ambacho wanaamini kitabadili eneo hilo.

Wetang’ula alitumia fursa hiyo kuhimiza kilimo cha pamba huku akishauri wakulima watumie mbegu mpya za zao hilo ambazo zitahakikisha mazao bora.

Huku akitambua kwamba mji wa Busia ni wa mpakani, Spika huyo alihimiza wakazi kufanya biashara hadi nchi jirani kama njia moja ya kujiongezea mapato.

Viongozi wengine waliohudhuria kikao hicho ni pamoja na Ferdinand Wanyonyi ambaye ni mbunge wa Kwanza, katibu wa viwanda Juma Mukhwana, wawakilishi wadi kadhaa na wazee wa jamii.

Website |  + posts
Share This Article