Eneo ambalo limejitenga la Somaliland limefungua ubalozi wake jijini Jerusalem nchini Israel, miezi 6 baada ya Israel kuwa taifa la kwanza kutambua eneo hilo kama taifa huru.
Hata hivyo, Somalia kupitia Wizara ya Mambo ya Nje imelaani hatua hiyo ikisema imekiuka sheria ya kimataifa.
Ubalozi huo ulifunguliwa wakati Rais wa Somaliland Abdirahman Mohamed Abdullahi alifanya ziara nchini Israel.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alifanya mashauriano na Abdullahi, akizungumzia uhusiano thabiti baina ya raia wa Israel na eneo la Somaliland.
Netanyahu alisifia hatua ya Somaliland kufungua ubalozi wake jijini Jerusalem badala ya jiji kuu la Tel Aviv ambako balozi za mataifa mengi zipo.
Mataifa kadhaa yakiwemo China, Uturuki, Saudi Arabia na Umoja wa Afrika (AU), zimeshtumu Israel kwa kuitambua Somaliland kama taifa huru, licha ya kwamba pande hizo mbili zimekuwa zikiboresha ushirikiano wao.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel Gideon Saar, mapema mwaka huu alizuru mji mkuu wa Somaliland, Hargeisa.
Eneo la Somaliland limejitawala tangu mwaka wa 1991 kufuatia kusambaratika kwa serikali kuu ya Somalia.
Eneo hilo limekuwa likiandaa uchaguzi binafsi, kubuni sarafu yake, vikosi vya ulinzi na limekuwa thabiti.