Mwanamuziki wa Marekani Snoop Dogg ametangaza kufutiliwa mbali kwa tamasha la Hollywood Bowl kutokana na mgomo unaoendelea hivi sasa wa waandishi wa miswada ya filamu kupitia chama chao cha Writers Guild of America – WGA na waigizaji wa vipindi vya runinga na wasanii wa runinga na redio nchini Marekani kupitia chama chao cha Screen Actors Guild – American Federation of Television and Radio Artists – SAG-AFTRA.
Snoop alitangaza hayo Jumanne kupitia mitandao ya kijamii ambapo aliandika, “Tunasikitika kuwafahamisha kwamba kutokana na mgomo unaoendelea na kwa sababu hatujui utaisha lini, tunahitaji kufutilia mbali onyesho la Hollywood Bowl”. Tamasha hilo lilikuwa limepangiwa kuandaliwa tarehe 20 mwezi Oktoba mwaka huu wa 2023.
Aliongeza kusema kwamba wanaunga mkono ndugu na dada wanachama wa WGA na SAG/AFTRA wakati huu mgumu wakitumai kwamba watayarishaji filamu kupitia muungano wao wa Alliance of Motion Picture and Television Producers – AMPTP wataridhia na kurejelea majadiliano.
Hatua ya Snoop ya kufutilia mbali tamasha la Los Angeles pekee na kukosa kugusia matamasha mengine ambayo amepanga katika sehemu nyingine nchini Marekani ni ujumbe kwa tasnia nzima ya Hollywood. Huenda ataendelea na matamasha ya maeneo mengine jinsi yalivyopangwa kwa sababu hajasema lolote kuyahusu.
Snoop ni mwanamuziki na kamwe hahusiki na mgomo unaoendelea wa wadau katika sekta ya filamu lakini anaonekana kuelewa kabisa wanayopitia.