Gachagua: Sing’atuki ng’o!

Dismas Otuke
1 Min Read
Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Niabu Rais Rigathi Gachagua amekanusha na kuondoa uwezekano wa kujiuzulu kutoka afisini, akielezea imani yake ya kushinda madai ya ufisadi yaliyowasilishwa dhidi yake mbele ya bunge la kitaifa.

Gachagua akihutubia taifa kutoka afisini mwake mtaani Karen Jumatatu jioni, aliapa kukabiliana na hoja iliyowasilishwa ya kutaka kumbandua, atakapofika bungeni kujitetea Jumanne kati ya saa kumi na moja jioni na saa moja usiku.

Naibu Rais alisema kamwe hatawahujumu Wakenya milioni saba waliomchagua wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2022 kwa kujiuzulu, huku akidokeza kujitetea katika mabunge yote mawili na kutarajia kupata haki.

Alisema madai yote yaliyowasilishwa katika bunge la taifa na mbunge wa Mwingi Magharibi Mutuse Mwengi hayana msingi wowote, akiyataja hujuma ya kumharibia sifa yeye na familia yake.

” Sina makosa dhidi ya madai hayo yote. Madai hayo yote hayajaafikia kiwango cha kuiniondoa mamlakani. Nitafika bungeni Jumanne saa kumi na moja jioni,” alisema Gachagua.

Madai yaliyowasilishwa dhidi ya Gachagua ni pamija na ukiukaji wa katiba, ulanguzi wa pesa, utovu wa maadili, kujihusisha na ufisadi, miongoni mwa mengine.

Share This Article