Simba wa milima ya Atlas waporomosha nyota ya Wabongo AFCON

Dismas Otuke
1 Min Read

Simba wa milima ya Atlas, Morocco wamefungua kindumbwendumbwe cha AFCON kwa moto na radi baada ya kuititiga Taifa Stars kutoka Tanzania mabao matatu kwa ombwe.

Mgaragazano huo wa ufunguzi kundi F umesakatwa Jumatano jioni katika kiwara cha Laurent Pokou mjini San Pedro nchini Ivory Coast.

Morocco walifungua karamu ya magoli kunako kipindi cha kwanza nahodha Romain Saiss, akifyatua kombora akiunganisha mkwaju wa adhabu uliochongwa na Hakim Ziyech.

Majirani walizidi kuhangaika zaidi kunako dakika ya 70 baada ya beki Novetus Miroshi kupigwa kadi nyekundu baada ya kulishwa njano mbili na kusalia wanandinga 10 uwanjani.

Azzedine Ounahi alitanua uongozi kwa vijana wa kocha Walid Regragui kwa bao la pili, kabla ya Yousef En Nesyri kukomelea msumari wa mwisho kwa jeneza la Taifa Stars.

Tanzania wanasalia bila ushindi tangu walipofuzu kwa michuano ya AFCON tokea mwaka 1980.

Website |  + posts
Share This Article