Sikukuu ya Mashujaa: Burudani ya kikamba

Marion Bosire
4 Min Read

Kama ilivyo ada, burudani huwa sehemu kubwa ya maadhimisho yote ya sikukuu za kitaifa na haikuwa tofauti katika uwanja wa Ithookwe kaunti ya Kitui, kulikoandaliwa sherehe za Mashujaa za mwaka huu wa 2025.

Baada ya Rais William Ruto kuwasili uwanjani humo dakika chache kabla ya saa nne asubuhi, akazunguka uwanja kusalimia wananchi na kukagua gwaride la heshima, burudani iliandaliwa.

Kwanza ilikuwa zamu ya jeshi la wanaanga kuonyesha vifaa vyao vya kazi na weledi wao katika kurusha ndege ambazo huwa zinatumika wakati wa dharura za kiusalama.

Lakini katika maonyesho hayo kwa wakati mmoja, wananchi walishtuliwa na mlipuko kutoka angani ambao mfawidhi alifafanua ni mlio wa uhuru.

Wanaskauti wa kike na kiume pia waliandaa gwaride la heshima mbele ya jukwaa la Rais, wakifuatiwa na wanachama wa St. Johns Ambulance huku bendi ikifunga gwaride hilo.

Watoto 520  wanafunzi wa shule mbalimbali za msingi katika kaunti ya Kitui nao waliandaa burudani fupi iliyoambatana na mada ya sherehe za mwaka huu ambayo ni “Kuwekeza katika kawi kwa ajili ya mustakabali endelevu”.

Walianza kwa kuandika neno “Kitui” kwa kutumia miili yao huku wakifoka maneno ya kukaribisha Rais William Ruto, Mashujaa na wageni kwa jumla kwa kaunti hiyo.

La pili walilolifanya ni kuandika maneno “Nishati” na “Ustawi” ambayo ni muhimu kuambatana na mada ya sherehe za mwaka huu za Siku ya Mashujaa na kufoka maneno “Nishati, Ustawi, Ushujaa”.

Walichora kifaa cha kuzalisha umeme kutokana na upepo yaani “Windmill”, jua na mtambo wa kuzalisha umeme kutokana na miale ya jua almaarufu Solar, vitendo walivyoambatanisha na shairi fupi kuhusu jinsi umeme umeunganishwa hata katika maeneo ya mashinani.

Waliandika pia neno Mashujaa huku wakiwapongeza kwa mchango wao katika jamii kwa wimbo mfupi na shairi lililosema kwamba kila mmoja ni shujaa.

Marehemu Raila Odinga naye hakusahaulika kwenye burudani ya watoto hao ambapo waliimba wimbo mfupi wa kumtaka alale salama na shairi fupi kuhusu mazuri yake na atakavyokoswa na wengi huku wakiandika jina “Shujaa Raila”.

Waandalizi wa burudani walicheza video ya Raila akiimba wimbo alioupenda sana wa “Jamaican Farewell” wa Harry Belafonte huku hadhira ikiwa imenyamaza kimya.

Tume ya kudumu ya muziki ya Rais PPMC nayo ilikuwa imeandaa burudani ya muziki, iliyohusisha wanamuziki kadhaa wenyeji wa kaunti ya Kitui na hata kaunti jirani.

Waliotumbuiza ni pamoja na kwaya ya taasisi ya mafunzo ya ualimu ya Kitui kwa wimbo wao “Nguvu ya Mashujaa” na kundi la kitamaduni la Itumani Mwenyenyo kwa densi ya “Mukanda”.

Wanamuziki Musomesa Mwenee, Jay Lava Baibe, Sauti Isu, Muthengi Ndagara na Kasupuu Ka Kamutei nao waliimba wimbo wao wa pamoja uitwao “Kenya Twi Mbee” yaani “Kenya Tuko Mbele”.

Wimbo “Kenya Tumeimarika” uliimbwa na Justus Myello, Winnie Mutanu, Ann Kathy, Stephen Kasolo, Priscilla Nina, Stellar Mengele, Dr. Mbuvi na mkata mauno maarufu Ndeke Ya Muthanga.

Mahukum, Bosbo Mulwa, Marash Ma Mkorea, Kakongo Sisters, Franco na Kisassy Boys Band walitumbuiza kwa wimbo wao “Kenya Nituutete” na mwisho kabisa ni kundi la kitamaduni la Ngwani lililotumbuiza kwa densi ya “Itheke”.

Website |  + posts
Share This Article