Mataifa wanachama wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA yamepitisha azimo lililowasilishwa na Kenya na Tanzania kwa niaba ya nchi za bara Afrika, kwamba Julai 7 itakuwa Siku ya Kiswahili Duniani.
“Tunatangaza Julai 7 ya kila mwaka kuwa Siku ya Kiswahili Duniani, itakayoadhimishwa kila mwaka kuanzia 2024,” liliamua Baraza hilo.
Azimio hilo linatambua wajibu muhimu unaotekelezwa na lugha ya Kiswahili katika kuleta amani, umoja, maendeleo ya kijamii na kiuchumi, tofauti za utamaduni pamoja na kubuni uhamasishaji na kukuza mazungumzo miongoni mwa watu.
“Kwa kuzingatia kuwa Kiswahili ni miongoni mwa lugha 10 zinazozungumzwa na watu wengi zaidi duniani, ikiwa na wazungumzaji zaidi ya milioni 200, ikiwa ni lugha katika nchi nyingi za Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika pamoja na Mashariki ya Kati, na kutambua jukumu la lugha hiyo katika kukuza amani, umoja na tofauti za kitamaduni, kujenga ufahamu na kukuza mijadala miongoni mwa watu,” ilisema azimio hilo.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), awali liliadhimisha siku ya lugha ya Kiswahili Julai 7 kila mwaka kuanzia mwaka 2022.
Katika mkutano mkuu wa UNESCO ulioandaliwa Novemba 23, 2021, ulitangaza Siku ya Kiswahili Duniani iadhimishwe kila mwaka.
Kiswahili ni miongoni mwa lugha 10 zinazozungumzwa zaidi duniani, wengi wa wazungumzaji wakitoka bara Afrika.