Hali DRC: Uhuru alaani kuzinduliwa kwa muungano wa kijeshi

Martin Mwanje
2 Min Read

Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta amelaani vikali kubuniwa kwa muungano wa kijeshi na kisiasa unaolenga kumbandua mamlakani Rais wa Jamhuri ya Demokrasia ya Congo, DRC Felix Tshisekedi. 

Uhuru badala yake ameelezea kuunga mkono mazungumzo ya usitishaji mapigano yanayoongozwa na Marekani na anataka muda wa kufanyika kw amazungumzo hayo kuongezwa ili kuwezesha mchakato wa ukuzaji amani, kusitisha mauaji ya kinyama na kuteseka kwa watu mashariki mwa DRC.

“Rais wa zamani Uhuru Kenyatta, ambaye ni Mpatanishi wa mchakato wa Amani wa Nairobi unaoongozwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC alitazama kwa mshtuko na hofu kwa yaliyojiri Ijumaa iliyopita, Disemba 15, 2023 jijini Nairobi, ambapo watu wanaodai kupigania maslahi ya amani kuu na utulivu nchini DRC walianzisha tena muungano mwingine wa kisiasa na kijeshi ili kubadilisha hali halali ya kisiasa nchini DRC,” ilisema taarifa iliyopachikwa katika mtandao wa X wa Uhuru.

“Mpatanishi huyo analaani vikali hali hii, na hasa sifa yao ya kijeshi, na semi zao zilizoseheni cheche za kisiasa na uchokozi.”

Ijumaa wiki iliyopita, wanasiasa wakuu wa DRC na wawakilishi wa makundi kadhaa likiwemo lile la waasi la M23 ambao wameteka eneo kubwa Mashariki mwa DRC, walizindua muungano kwa jina “Congo River Alliance” jijini Nairobi.

Kulingana na mmoja wa wahusika, muungano huo unaleta pamoja makundi kadhaa yaliyojihami ya DRC, makundi ya kijamii na ya kisiasa.

Corneille Nangaa, ambaye aliwahi kuhudumu kama msimamizi wa Tume ya Uchaguzi nchini DRC, na ambaye aliwekewa vikwazo na Marekani kwa kuhujumu uchaguzi wa mwaka 2018 aliongoza uzinduzi huo.

Alisema lengo kuu ni kutafuta suluhisho la kudumu kuhakikisha watu wa DRC wanaishi pamoja kwa amani.

Walibuni muungano huo wakati ambapo DRC inajiandaa kwa uchaguzi wa urais na wa ubunge Disemba 20, 2023.

Kufuatia kuzinduliwa kwa muungano huo, serikali ya DRC imewaita mabalozi wake nchini Kenya na Tanzania kwa kile kilichotajwa kuwa kufanywa kwa majadiliano.

 

Share This Article