Mashindano ya Kitaifa ya michezo baina ya shule za upili (KSSSA),yatango’a nanga jumapili hii mjini kisii huku shule zilizofuzu kutoka kote nchini zikijiandaa vilivyo kushinda.
Michezo hiyo inajumuisha soka, raga ya wachezaji saba kila upande, tenisi ya meza,voliboli, vikapu ya 3×3, badminton na netiboli kwa wasichana.
Mwaka huu,mkoa wa pwani uliandaa mashindano yake mjini Hola kaunti ya Tana River kisha shule zifuatazo zikajikatia tiketi ya kitaifa.
Dr. Aggrey High na Kombani watawakilisha kwenye soka ya wavulana na wasichana mtawalia huku wavulana wa Malindi High na vipusa wa Paul Haris wakigaragaza raga.
Wavulana wa Milalulu watacheza voliboli pamoja na warembo wa Vyambani huku Mombasa Baptist ikijaza vikapu nayo Kaya tiwi ikitesa katika netiboli.
Shule hizo zilianza safari leo usubuhi kuelekea katika kipute hicho cha wiki ijayo kitakachosakatwa kwenye nyuga mbali mbali.
Mashabiki wa netiboli, vikapu, tenisi, badminton na raga watakita kambi katika shule ya Kisii na wa soka na voliboli wawe Mosocho na Cardinal Otunga High.
Mashindano hayo yataanza tarehe 4 hadi 8 na watakaong’aa watafuzu kwa kinyanganyiro cha Afrika Mashariki baina ya shule za pili mjini Mbale nchini Uganda mwezi huu.