Huenda shule na vyuo vya umma vikakosa kufunguliwa tena kwa muhula mpya mwezi huu baada ya walimu na wahadhiri kutishia kugoma.
Walimu na wahadhiri wamesema watagoma kote nchini endapo serikali haitatimiza matakwa yao ya nyongeza ya mishahara.
Tayari, vyama vya walimu vya KNUT na KUPPET vimetoa ilani ya mgomo sawia na chama cha wahadhiri wa vyuo vikuu, UASU.
Endapo tishio la migomo hiyo litatakelezwa, sekta ya elimu huenda ikalemazwa na kuathiri zaidi mitihani ya kitaifa ya KCSE na KCPE inayotarajiwa kuanza mwezi Oktoba.
Kwa upande mwingine, wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na vyuo vikuu mwezi ujao huenda wakasalia nyumbani kwa kipindi kirefu.
Waziri mpya wa Leba Dkt. Alfred Mutua tayari ameingia kati kujaribu kuzuia kufanyika kwa migomo hiyo ambayo madhara yake hayasemezeki.