Usimamizi wa chuo kikuu cha Moi, umetangaza kufungwa mara moja kwa chuo hicho, kutokana na mgomo unaoendelea wa wafanyakazi na ghasia za wanafunzi.
Kupitia taarifa iliyotiwa saini na naibu chansela wa chuo hicho Prof. Isaac Kosgey, alisema uamuzi huo umeafikiwa kufuatia mkutano maalum wa Seneti ya Chuo hicho ulioandaliwa leo Alhamisi.
Kosgey aliongeza kuwa shughuli za masomo za Muhula wa kwanza wa Mwaka wa Masomo wa 2024/2025 zimesitishwa, akisema tarehe mpya ya ufunguzi itawasilishwa kwa wakati ufaao.
“Wanafunzi wote katika mabewa yote ya chuo hiki, waondoke mara moja. Wanafunzi wote ambao ni raia kigeni kuwasiliana na mkuu wa kitivo,” ilisema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa baraza la usimamizi wa chuo hicho, unajizatiti kuhakikisha shughuli za kawaida zinarejelea hivi karibuni.
Wahadhiri wa chuo hicho wanataka kulipwa mishahara yao iliyocheleweshwa, pamoja na utekelezaji wa Makubaliano ya Pamoja (CBA).