Gavana wa kaunti ya Bomet Hillary Barchok na Gavana wa zamani wa kaunti ya Bungoma Wycliffe Wangamati wamejipata matatani wakati serikali ya Kenya Kwanza ikiimarisha vita dhidi ya ufisadi.
Hii ni baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), Renson Ingonga kuagiza kushtakiwa kwa wawili hao kutokana na tuhuma za ufisadi.
Ingonga amethibitisha kupokea faili ya uchunguzi kutoka kwa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi, EACC ikipendekeza kukamatwa kwa Gavana Barchok na Mkurugenzi wa kampuni ya Chemasus Construction Limited Evans Korir.
Mashtaka yanayowakabili ni pamoja na ulanguzi wa fedha, kujilimbikizia mali ya umma kwa njia ya ulaghai na mgongano wa maslahi miongoni mwa mengine.
Kwa upande wake, Wangamati pia anakabiliwa na mashtaka sawia ya mgongano wa maslahi miongoni mwa menngine.
Kwenye taarifa, Ingonga pia ameagiza uchunguzi zaidi kufanywa dhidi ya Magavana Kimani Wamatangi wa Kiambu na Mohammed Mahamud Ali wa Marsabit.
Wawili hao wanakabiliwa na mashtaka ya mgongano wa maslahi miongoni mwa mashtaka mengine.
Katika kesi inayomkabili Gavana wa Marsabit Mohamud, Ingonga alisema kuna mapungufu katika ushahidi ambayo yanahitaji kuangaziwa upya kwa uchunguzi zaidi.
Katika Kaunti ya Kiambu, faili ya uchunguzi kutoka kwa EACC imependekeza kushtakiwa kwa Gavana Kimani Wamatangi pamoja na watu wengine saba kwa kwa mgongano wa maslahi na kujipatia mali ya umma kinyume cha sheria.
DPP ametoa maagizo hayo wakati Rais William Ruto ameapa kukabiliana na vikali na zimwi la ufisadi nchini, na tayari amebuni timu inayozileta pamoja asasi mbalimbali za serikali kwa lengo la kuimarisha vita dhidi ya ufisadi.
Hata hivyo, mahakama imeizuia timu hiyo kutekeleza majukumu yake baada ya kesi kuwasilishwa ikihoji uhalali wake.