Shirika la KEPHIS laimarisha vita dhidi ya mbegu ghushi

Tom Mathinji
1 Min Read
Mwenyekiti wa KEPHIS Joseph M’uthari.

Shirika la Kutathmini Ubora wa Mbegu na Ustawishaji wa Mimea (KEPHIS), limeimarisha vita dhidi ya wauzaji wa mbegu ghushi kwa wakulima wasio na ufahamu.

Akizungumza jijini Mombasa, mwenyekiti wa KEPHIS Joseph M’uthari, alisema kuwa tayari washukiwa kadhaa wa biashara hiyo haramu wamekamatwa.

“Tuko mbioni kuhakikisha kuwa wakulima wanapata mbegu zinazofaa kwa msimu wa upanzi,” M’uthari alisema.

“Timu ya mawakala mbalimbali ilipata tani 18 za mbegu ghushi hasa za mahindi na kuwafungulia mashtaka watu 65 kote nchini.”

M’uthari alisema kuwa timu hiyo ya wakala inapania kuongeza idadi ya wafanyakazi zaidi ili kusaidia katika kukabiliana na uuzaji wa mbegu ghushi.

Alitoa wito kwa wakulima kununua mbegu katika maduka yaliyo na leseni rasmi ya shirika la KEPHIS ili kuepukana na kulaghaiwa.

Vita hivi vinaendelea kuchacha ikiwa tayari mbegu ghushi zimepatikana zikiuzwa kwenye kaunti za Kisii, Nyamira, Nakuru, Nzoia, Elgeyo Marakwet, Makueni, Kericho, Bomet, Kajiado, Nairobi, Bungoma, Kiambu na Murang’a.

TAGGED:
Share This Article