Shirika la KBC kushirikiana na lile la Xinhua kuimarisha utoaji habari

Tom Mathinji
1 Min Read

Serikali ya Kenya kupitia shirika la utangazaji nchini KBC, inatafuta fursa za ushirikiano na shirika la habari la kiserikali nchini China la Xinhua, kwa mujibu wa Naibu rais Rigathi Gachagua.

Naibu rais alisema huku serikali ikiimarisha shirika la KBC ili liwe la kisasa, ushirikiano na shirika la Xinhua utakuza uhamishaji wa maarifa na ujuzi kando na kuimarisha juhudi za kuelezea taarifa kuhusu fursa za kiuchumi katika nchi hizi mbili.

Alisema ushirikiano na shirika la Xinhua utaimarisha zaidi uhusiano baina ya nchi hizi mbili uliodumu kwa miaka 60

“Tunalenga kuimarisha shirika la utangazaji nchini KBC, ili liwe kituo dhabiti zaidi katika kuwafahamisha wakenya,”alisema Gachagua.

Kwa upande wake rais wa shirika la habari la Xinhua, Fu Hua, alisema shirika hilo liko tayari kushirikiana na KBC katika  utumizi wa teknolojia mpya  na uvumbuzi.

Maeneo ya ushirikiano ni pamoja na uwekezaji na sekta ya utalii miongoni mwa mengine.

Balozi wa China humu nchini Zhou Pingjian na kaimu mkurugenzi wa KBC Samuel Maina, walihudhuria mkutano huo.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *