Msanii maarufu wa muziki, Zuwena Mohamed maarufu kama Shilole, ameadhimisha miaka 10 ya mafanikio yake katika biashara ya chakula kwa tukio la kipekee lililofanyika Mikocheni, Dar es Salaam.
Msanii huyo wa muziki alikuwa anasherehekea miaka 10 ya hoteli yake maarufu ya Shishi Food.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na wadau mbalimbali wa sanaa, wakiwemo wasanii wakubwa kama Diamond Platnumz, pamoja na viongozi wa sekta ya sanaa.
Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu Mtendaji wa BASATA, Dkt. Kedmon Mapana, alimpongeza Shilole kwa juhudi zake za kukuza tasnia ya sanaa na ujasiriamali.
Dkt. Mapana alisisitiza umuhimu wa wasanii kuwa na maadili, kushirikiana na kutumia vipaji vyao kuboresha maisha yao na jamii kwa jumla.
Aidha, Dkt. Mapana alikumbusha wasanii kuhusu fursa ya kipekee ya kupima magonjwa ya moyo katika Hospitali ya Moyo ya Jakaya Kikwete kila Jumamosi na Jumapili ya mwezi huu wa Disemba.
Alieleza kuwa huduma hiyo ni ya bure kabisa bila malipo na inalenga kusaidia wasanii kutambua hali ya afya zao mapema na kuchukua hatua stahiki.
“Ninawasihi wasanii wote, pamoja na wadau wa sanaa, kuitumia fursa hii ya kupima afya zenu. Afya bora ni msingi wa mafanikio katika sanaa na maisha kwa ujumla,” alisema Dkt. Mapana.
Kwa upande wake, Shilole aliwashukuru mashabiki na wadau wa sanaa kwa kumuunga mkono katika safari yake ya muziki na ujasiriamali.
Alisema miaka 10 ya mafanikio yake ni ushahidi wa bidii, nidhamu, na kujituma kwake, huku akihamasisha wasanii wengine kuwekeza zaidi katika kazi zao na maisha yao binafsi.
Tukio hilo liliambatana na burudani za muziki, hotuba za hamasa, likiwa ni mfano wa mshikamano na mafanikio yanayopatikana kupitia ushirikiano katika tasnia ya sanaa.