Serikali imetangaza kutekelezwa kikamilifu kwa sheria na masharti yanayodhibiti sekta ya kilimo kote nchini.
Zoezi hilo linalotekelezwa na wizara ya usalama, litahusisha wizara ya kilimo na ustawi wa mifugo, wizara ya afya na serikali za kaunti.
Akizungumza katika taasisi ya mafunzo ya serikali wakati wa mkutano wa hali ya juu ulioleta pamoja asasi za usalama kabla ya kuanza kutekelezwa kwa zoezi hilo, Katibu katika wizara ya usalama wa taifa Dkt.Raymond Omollo, alisema kumekuwa na ongezeko la visa vya wizi wa mifugo, biashara ambayo haijadhibitiwa ya bidhaa za mifugo na uuzaji wa chakula ambacho hakijakaguliwa na kusababisha maafisa hapa nchini.
“Tunashuhudia pia wizi wa mifugo katika maeneo ya Rift Valley, Mashariki na katikati mwa nchi, huku wakisafirishwa Nairobi na katika maeneo mengine. Wizi huu wa mifugo unahusishwa na kuibuka kwa ujangili na wezi wa mifugo wanaouza nyama ya mifugo hao kwa wafanyabiashara na makundi ya majangili ambao huuza bidhaa za mifugo kama vile ngozi katika maeneo yanayohusiahwa na biashara haramu ya wanyamapori,” alisema Katibu huyo
Makamishna wote wa kaunti wameagizwa kubuni vikosi vya asasi mbalimbali vinavyojumuisha maafisa wa polisi, wale wa ujasusi, maafisa wa serikali ya taifa, maafisa wa afya ya umma na maafisa wa matibabu ya mifugo pamoja na kuhusisha mashirika ya kudhibiti kwa lengo la kuhakikisha sheria hizo zimetekelezwa.
Maafisa hao wa asasi mbali mbali wanapaswa kutambua maeneo maafuru yanayotumiwa kuwachinja mifugo kinyume na sheria,kuwatia nguvuni wahusika pamoja na kusambaratisha magenge ya wahalifu yanayohusika.
Kwa upande wake, Katibu katika idara ya ustawi wa mifugo Jonathan Mueke, alisema “Tumeshuhudia mianya katika sheria za kudhibiti sekta ya mifugo na tumebuni mikakati inayolenga vituo vya kushughulikia bidhaa za mifugo pamoja na usafiri,”.
Mueke alitoa wito kwa maafisa hao wa asasi mbali mbali kutekeleza majukumu yao kikamilifu kutekeleza sheria hizo, huku akipongeza mchango wa Makamishna wa kaunti na wale wa kanda.
Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Mkurugenzi wa upelelezi wa jinai Mohamed Amin, Mkurugenzi wa afya ya umma Dkt.Maureen Kamene, Makamishna wa kanda, Makamishna wa kaunti, makamanda wa polisi na washikadau katika sekta ya mifugo