Sheria ya walemavu kurekebishwa ili kuwapendelea zaidi

Marion Bosire
1 Min Read

Waziri wa Leba na Utunzi wa Jamii Florence Bore amesema kwamba wizara yake imekuwa ikitekeleza mipango kadhaa ya kuboresha maisha ya walemavu kama vile marekebisho kwa sheria ya walemavu ya mwaka 2003.

Bore ambaye aliongoza maadhimisho ya Siku ya Walemavu Duniani katika kaunti ya Pokot Magharibi jana Jumapili alisema marekebisho mengine ni kujumuisha walemavu zaidi kwenye mpango wa “Inua Jamii”.

“Tujitahidi kuhakikisha ulimwengu unaotizama ulemavu sio kama kikwazo bali kama sifa za kipekee ambazo zinaweza kuwa muhimu ikiwa watu hao watapatiwa fursa faafu,” alisema Waziri Bore.

Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni “Kuungana katika juhudi kuokoa na kuafikia malengo ya maendeleo endelevu kwa ajili ya walemavu, pamoja na walemavu na kupitia kwa walemavu”.

Bore alisema kauli mbiu hiyo inasisitiza jukumu muhimu ambalo malengo ya maendeleo endelevu yanatekeleza katika kupunguza ukosefu wa usawa kwa kuhakikisha haki za kijamii, kiuchumi na kisiasa kwa wote.

Wizara hiyo ya utunzi wa jamii imeahidi kusajili walemavu wapatao 137,119 kwenye mpango wa Inua Jamii ambapo watapata pesa za kujikimu kila mwezi.

Hata hivyo, alifafanua kwamba uchunguzi zaidi utatekelezwa ili kuhakiki ufaafu wa watu hao kupokea pesa kutoka kwa serikali.

Share This Article