Watoto wawili wameuawa na tisa kujeruhiwa vibaya huku sita wakiwa hali mahututi katika shambulio la kisu kwenye warsha ya watoto kucheza densi.
Watu wazima wawili pia wako katika hali mahututi baada ya kudungwa visu walipokuwa wakijaribu kuwalinda watoto katika hafla iliyokuwa imepewa jina Taylor Swift kwenye Mtaa wa Hart huko Southport, Polisi wa Merseyside walisema.
Mvulana mwenye umri wa miaka 17, kutoka Banks huko Lancashire, amekamatwa kwa tuhuma za mauaji na jaribio la kuua.
Polisi walisema sababu ya shambulio hilo “haikuwa wazi” lakini haikuchukuliwa kama yenye kuhusishwa na ugaidi.
Shahidi mmoja alielezea tukio hilo kama “la kutisha” na akasema “hawajawahi kuona kitu kama hicho”.
Mfalme na waziri mkuu wameongoza kwa salamu za rambirambi kwa wale walioathiriwa.
Polisi wa Merseyside walitangaza kutokea kwa tukio kubwa baada ya kupokea simu za dharura saa 11.47 saa za eneo, wiki ya kwanza ya likizo za shule wakati wa majira ya joto kwa watoto wengi nchini Uingereza.
Magari ya kujihami, ya kubeba wagonjwa 13 na zima moto walikimbilia eneo la tukio ambapo tamasha la watoto wenye umri wa miaka 6 hadi 10 lilikuwa likifanyika.