Aliyekuwa Setter wa timu ya taifa ya Voliboli kwa vidosho Janet Wanja, amefariki jana usiku akiwa na umri wa miaka 40 baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Kulingana na taarifa kutoka kwa familia, Wanja amekuwa akipokea matibabu ya saratani ya kibofu cha nyongo.
Familia hiyo kupitia kwa mchezaji soka Kevin Kimani ambaye ni kakake Wanja, imetoa shukrani kwa kampuni ya Kenya Pipeline kwa kusimama na marehemu ambaye alikuwa akiichezea zamani na kulipa gharama ya matibabu, shirikisho la mpira wa wavu nchini KVF, kamati ya Olimpiki nchini ,NOC-K na shirikisho la kandanda nchini, FKF, kwa kumsaidia wakati wa kuugua kwake.
Wanja alizaliwa Februari 24 mwaka 1984 na alianza amali yake ya voliboli akiwa katika shule ya wasichana ya Mukumu, kabla ya kujiunga na vilabu vya Kenya Commercial Bank na Kenya Pipeline.
Wanja atakumbukwa kwa kuichezea timu ya taifa ya Kenya-Malkia Strikers katika michezo ya Olimpiki ya mwaka 2000 mjini Sydney ,Australia na 2004 mjini Athens Ugiriki, kabla ya kuisaidia Kenya kutwaa ubingwa wa Afrika kwa mara ya saba mwaka 2007, akitawazwa Setter bora wa mashindano hayo.
Mwaka huu, Wanja alikuwa katika dawati la kiufundi la Malkia Strikers iliposhiriki michezo ya Olimpiki jijini Paris, Ufaransa.
Mola ailaze roho yake mahali pema penye wema.