Serikali yawekeza shilingi bilioni 3.5 kuimarisha sekta ya Majani Chai

Tom Mathinji
1 Min Read
Wakulima wa Majani Chai kupata mapato yaliyoimarika.

Wakulima wa Majani Chai hapa nchini, wanatarajia mapato yaliyoimarika baada ya hatua ya serikali ya kuwekeza shilingi bilioni 3.5 kuimarisha viwanda vya Majani Chai kufikia viwango vya kimataifa.

Akizungumza katika kiwanda cha Majani Chai cha  Olenguruone wakati wa hafla ya kutoa cheti cha ushirika cha kiwanda hicho, Katibu katika Wizara ya Kilimo Dkt. Kipronoh Ronoh, alidokeza kuwa serikali imeweka mbele masilahi ya wakulima huku akiwaonya wasimamizi wa Halmashauri ya Maendeleo ya Majani Chai (KTDA) dhidi ufisadi na kufuja fedha za viwanda hivyo.

Kulingana na Dkt. Ronoh, wakulima sasa watalipwa shilingi 26 kwa kilo moja ya Majani Chai, hii ikiwa ni ongezeko kutoka shilingi 16 kwa kila kilo.

“Serikali ya Kenya inatekeleza mageuzi kuimarisha sekta ya Majani Chai, kwa lengo la kuongeza mapato kwa wakulima hadi shilingi 100 kwa kilo moja ya zao hilo kufikia mwaka 2027 kupitia kukabiliana na gharama ya juu ya uzalishaji na uongezaji dhamani,” alisema Dkt. Rono.

Dkt. Ronoh alisema fedha hizo zitatumika kuboresha viwango vya viwanda 19 vya Majani Chai ili kuhakikisha vinafikia viwango vya juu na kupunguza gharama ya uzalishaji.

Aidha alitoa changamoto kwa viwanda vya bidhaa hiyo kukumbatia uongezaji dhamani ili kufika viwango vya soko la kimataifa.

Share This Article