Naibu Rais Rigathi Gachagua amewahakikishia wakulima wa kahawa juu ya kupatikana kwa suluhu kwa changamoto za kifedha zinazowakumba ikiwa ni pamoja na uwezekano wa kufutilia mbali madeni yao.
Amesema serikali haitalegea katika kutekeleza mageuzi yanayoendelea katika seka ya kilimo, akiongeza kuwa serikali inachukua hatua zaidi za kuongeza mapato ya wakulima wa kahawa.
Hakikisho la Naibu Rais linakuja baada ya baadhi ya viongozi kutoa wito kwa serikali kufutilia mbali madeni ya wakulima.
Akiwahutubia mamia ya wakulima wa kahawa leo Jumatano katika eneo la Maragua, kaunti ya Murang’a baada ya kuzindua kiwanda cha kusaga kahawa cha Murang’a, Gachagua alisema serikali ya Kenya Kwanza inashughulikia suala hilo.
“Mimi mwenyewe na Mawaziri Prof. Njuguna Ndung’u wa Fedha na Simon Chelugui wa Vyama vya Ushirika tutaangazia suala la madeni na kupata suluhu,” alisema Naibu Rais.
Wakulima wa kahawa wanadaiwa madeni hayo na wakopeshaji wa fedha na wanunuaji wa zao hilo.
Gachagua akiongeza kuwa serikali imewashinda matapeli na mawakala waliokuwa wakiwapunja wakulima katika sekta ya kahawa.
“Niliagizwa na Rais William Ruto kuongoza mageuzi katika sekta ya kahawa na tunaendelea vizuri. Tumekabiliana na kuwashinda matapeli na mapato yanayotokana na uuzaji wa kawaha nje ya nchi yameongezeka maradufu katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita,” aliongeza Naibu Rais.