Serikali inafadhili jumla ya miradi 1,200 ya thamani ya shilingi bilioni 18 kutoka kwa hazina ya usawazishaji, ambayo hugawiwa kaunti 33.
Akizungumza leo kwenye kongamano la viongozi wa jamii za wafugaji katika kaunti ya Wajir, Rais William Ruto alisisitiza kujitolea kwa serikali kuhakikisha kwamba hazina hiyo inasuluhisha tofauti za kimaeneo katika maendeleo.
Kiongozi wa nchi alisema anatumai hazina hiyo pia itahimiza ukuaji jumuishi katika maeneo yaliyoachwa nyuma kimaendeleo nchini Kenya.
Hazina ya usawazishaji hutengewa asilimia 0.5 ya mapato jumla ya serikali ya taifa kila mwaka ili kufadhili utoaji huduma za kimsingi katika maeneo yaliyotengwa.
Rais vile vile alihakikishia jamii za wafugaji kwamba mpango wa urejesho wa mifugo walioangamia kwa wingi wakati wa kiangazi mwaka jana unaendelea.
Kulingana naye mpango huo unalenga kufaidi familia elfu 10.
Kuhusu chanjo ya mifugo, Rais Ruto alisema itaanza kutolewa kote nchini mwezi Januari mwaka ujao wa 2025. Aliwasuta wanaoeneza habari za uongo kuhusu mpango huo akisema unalenga kulinda afya ya mifugo na kuhakikisha usalama wa chakula.
Mpango huo unalenga ng’ombe milioni 22 watakaochanjwa dhidi ya ugonjwa wa miguu na midomo huku mbuzi na kondoo milioni 50 wakichanjwa dhidi ya ugonjwa wa Peste des Petits Ruminants (PPR).
Rais alisema kwa kuzuia magonjwa ya mifugo, Kenya itaweza kujihakikishia soko la bidhaa za mifugo kimataifa.
Aliongeza kusema kwamba dawa zitakazotumiwa katika mpango huo wa chanjo ya mifugo zitatengenezewa humu nchini.