Serikali yatenga fedha zaidi za ununuzi wa mbolea

Tom Mathinji
2 Min Read

kiwango cha uzalishaji wa chakula hapa nchini kinatarajiwa kuongezeka,  kufuatia hatua ya serikali ya kuongeza bajeti yake kwa mbolea ya ruzuku.

Katika mswada wa makadirio ya bajeti ya ziada (Nambari.3) ambao ulitiwa saini na Rais William Ruto katika ikulu ya Nairobi siku ya Alhamisi, shilingi bilioni 8.25 zimeongezwa kwa ununuzi wa mbolea.

Ili kudhibiti hasara na kuhakikisha kuimarika kwa bei ya mahindi nchini, shilingi bilioni 2.1 zimetengewa usimamizi wa baada ya mavuno.

Serikali inasema matumizi ya fedha hizo yatajumuisha ununuzi wa vifaa vya kukausha mahindi, maghala makubwa-makubwa na ukiwemo ununuzi wa mahindi zaidi kutoka kwa wakulima ili kuwaepusha na mfumko wa bei.

Serili imesema itanunua zao hilo kutoka kwa wakulima shilingi 4,000 kwa kila gunia la kilo 90.

Aidha, shilingi bilioni 1.7 zaidi zimetengewa mageuzi na mabadiliko yanayoendelea kutekelezwa katika sekta ya sukari,yakiwemo malimbilizi ya malipo kwa wakulima na kuimarisha ukolevu wa kiwango cha utamu wa sukari.

Ili kuimarisha uzalishaji wa kahawa nchini, serikali imetenga shilingi bilioni 4 kwa ajili ya ufufuzi wa sekta hiyo.

Kiongozi wa wengi Kimani Ichungw’ah alisema shilingi milioni 400 zimetengewa shirika la New KCC, kununua maziwa ya ziada wakati huu wa msimu wa mvua.

“Hatua hii itahakikisha wakulima hawapati hasara kutokana na ongezeko la maziwa katika soko,” alisema Ichung’wa.

Share This Article