Serikali yatangaza msako wa kitaifa dhidi ya pombe haramu

Tom Mathinji
1 Min Read
Waziri wa usalama wa taifa Prof. Kithure Kindiki atoa agizo la msako dhidi ya Pombe haramu.

Waziri wa usalama wa kitaifa Prof. Kithure Kindiki, ameagiza kutekelezwa kwa msako wa kitaifa dhidi ya pombe haramu.

Agizo hilo la Kindiki, linajiri wiki moja baada ya watu 17 kufariki katika kaunti ya Kirinyaga baada ya kubugia pombe haramu.

Akizungumza baada ya kushiriki mazungumzo na kamati za usalama  na ujasusi za kaunti ya Kirinyaga na kaunti ndogo ya Mwea Magharibi, waziri huyo aliagiza kamati za usalama katika kaunti zote 47 kutekeleza agizo hilo kikamilifu.

“Sehemu zote za kuuza pombe haramu sharti zifungwe, na wamiliki wachukuliwa hatua za kisheria,” alisema Kindiki.

Kulingana na waziri huyo, utengenezaji na uuzaji wa pombe haramu utakabiliwa vilivyo sawia na vita dhidi ya ugaidi, wizi wa mifugo na uhalifu mwingine wa kiwango cha juu.

Kindiki alidokeza kuwa serikali imezindua mpango wa urekebishaji tabia, huku akiwaagiza machifu na manaibu wao kukusanya takwimu kutoka kila kijiji, ili waathiriwa wasaidiwe kupitia mpango huo.

Aliwaonya maafisa wa usalama na wale wa serikali watakaopatikana wakifanikisha utengenezaji, uuzaji, unywaji wa pombe haramu, mihadarati au bidhaa zingine zilizoharamishwa, ataachishwa kazi na kufunguliwa mashtaka.

Share This Article