Viongozi wa dini ya Kiislamu wamelaani utumizi wa nguvu kupita kiasi, uliotekelezwa na maafisa wa polisi walipokuwa wakidhibiti maandamano dhidi ya serikali.
Kupitia kwa taarifa leo Alhamisi, viongozi hao walitoa wito kwa Rais William Ruto kuchukua hatua dhidi ya ukatili wa polisi na visa vya utekaji nyara.
“Kama ishara ya uongozi na uzalendo, tunakusihi kuwachukulia hatua maafisa wa polisi wakatili, na kuzuia utekaji nyara wa waandamanaji,” ilisema taarifa hiyo.
Wakati huo huo viongozi hao walitaka kuachiliwa huru kwa waandamanaji wanaozuiliwa katika vituo vya polisi, na kufidiwa kwa wale waliolazwa hospitalini pamoja na kusaidia familia zilizowapoteza jamaa zao.
Aidha viongozi hao waliojumuisha wale wa Baraza Kuu la Waislamu nchini (SUPKEM), kongamano la kitaifa la viongozi wa Kiislamu (NAMLEF), na Baraza la Maimamu na Wahubiri wa Kenya (CIPK), walielezea wasiwasi wao kuhusu visa vya ghasia na utovu wa usalama unaoongezeka nchini, huku wakitoa wito wa kutekelezwa kwa mbinu mpya kukabiliana na changamoto zinazokumba taifa hili.
“Vijana wanataka hatua kuchukuliwa kuhusu maswala waliyoibua. Hawana haja na mazungumzo kuhusu mambo ambayo unayoweza tekeleza kupitia mfumo wa sheria na katiba,” walisema viongozi hao.