Makundi yanayoshinikiza kudumishwa kwa usalama barabarani humu nchini yanaitaka serikali kutangaza ajali zinazoongezeka barabarani kuwa janga la kitaifa.
Aidha, yanaitaka serikali kuchukua hatua za haraka ili kudhibiti vifo vinavyotokana na ajali hizo, ikiwa ni pamoja na kuifanyia mabadiliko Mamlaka ya Taifa ya Uchukuzi na Usalama Barabarani (NTSA).
Wakiongozwa na mwenyekiti wa Chama cha Vidhibiti Mwendo na Usalama Barabarani Edward Gitonga, maafisa wa makundi hayo pia wamemtaka Waziri wa Barabara na Uchukuzi Davis Chirchir kuwaleta pamoja washikadau katika sekta hiyo kwa lengo la kutafuta njia bora za kukomesha maafa barabarani.
Gitonga alitoa wito wa maafisa wote wa ngazi za juu wa NTSA kusailiwa upya akidai wengi wao hawastahili kushikilia nyadhifa hizo.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa chama hicho John Mutisya alisema vifo vinavyotokana na ajali barabarani vinaweza vikapunguzwa kwa nusu katika kipindi cha takriban miezi sita ikiwa Chirchir atafanya kazi na washikadau yakiwemo makundi ya usalama barabarani kukabiliana na hali hiyo.
Mwenyekiti wa Chama cha Usalama Barabarani nchini Kenya David Kiarie alitoa wito kwa Wizara ya Barabara na Uchukuzi kuondoa maafisa wa NTSA barabarani kwa madai ya utepetevu kama ilivyoshuhudiwa wakati wa msimu wa sherehe.
Badala yake, Kiarie anataka nafasi ya maafisa hao kuchukuliwa na polisi wa trafiki.
Taarifa ya Antony Musyoka