Serikali yatakiwa kufafanua kuhusu hifadhi ya miili ya Shakahola

Seneta wa Kilifi anataka kujua ni kwa nini miili hiyo imeendelea kuwekwa kwenye hifadhi iliyokusudiwa kuwa ya muda mfupi.

Marion Bosire
2 Min Read

Seneta wa kaunti ya Kilifi Stewart Madzayo ameitaka Serikali kutoa maelezo ya kina kuhusu kuendelea kuhifadhiwa kwa miili ya waathiriwa wa janga la Shakahola.

Akiwasilisha ombi katika Bunge la Seneti, Seneta Madzayo aliashiria kuwa suala hilo limekuwa chanzo cha taharuki na hatari za kiafya kwa wakaazi na wahudumu wa hospitali ya Kata Ndogo ya Malindi ambapo miili hiyo imehifadiwa kwenye makontena ya muda.

“Ni jambo la kusikitisha kwamba, licha ya ufukuaji wa miili na tafiti za DNA zilizofanywa na serikali, miili ya waathiriwa immendelea kuhifadhiwa kwenye makontena ya muda katika Hospitali ya Kata Ndogo ya Malindi,” alilalama.

Aliongeza kwamba familia za waathiriwa hao bado hazijapata nafasi ya kupumzisha wapendwa wao, miaka mitatu baada ya janga la Shakahola.

Katika ombi lake, Seneta Madzayo aliitaka Kamati ya Usalama wa Taifa, Ulinzi na Mahusiano ya Kigeni kubaini idadi ya miili ya waathiriwa wa Shakahola inayohifadhiwa katika makontena ya muda ya Hospitali ya Kata Ndogo ya Malindi.

Kamati hiyo inahitajika pia kutoa sababu za kucheleweshwa kwa mchakato wa utambuzi wa miili, hali ambayo kulingana na Seneta huyo, imezuia familia kupata hitimisho na kuandaa mazishi ya wapendwa wao.

Kiongozi huyo wa wachache kwenye Seneti aidha aliitaka kamati hiyo chini ya uongozi wa Seneta wa Isiolo Fatuma Dullo kufafanua hatua zilizochukuliwa na serikali kuharakisha utambuzi, vipimo vya DNA na msaada kwa familia zilizoathirika.

Kadhalika, aliitaka kubaini ratiba ya muda wa kukamilisha utambuzi wa miili ili kuruhusu mazishi ya waathiriwa wa janga la Shakahola.

Share This Article