Mchakato wa kuchagua Papa mpya huwa umeghubikwa na usiri mkubwa, ambapo wahusika hufungiwa kabisa katika eneo moja hadi uamuzi uafikiwe.
Baada ya Papa Francis, kuaga dunia Aprili 21, 2025, sasa msako wa kutafuta kiongozi mpya wa Kanisa Katoliki ulimwenguni, ambalo lina waumini zaidi ya bilioni 1.3 unanukia.
Kwa kawaida kazi hiyo huanza katika muda wa siku 15 hadi 20 baada ya kifo au kujiuzulu kwa Papa aliye mamlakani na walio na mamlaka na jukumu la kuchagua Papa ni makadinali wakuu.
Makadinali hao huwa katika sehemu mbali mbali ulimwenguni na muda huo wa siku 15 hadi 20 ni wa kuwaruhusu kusafiri hadi Vatican, Roma kwa shughuli hiyo muhimu.
Mkutano wa kisiri wa kutafuta Papa mpya unaohusisha baraza la makadinali au college of cardinals hufahamika kama “Conclave” kwa kiingereza.
Aliyehitimu kuwa Papa ni kiumbe yeyote wa kiume ambaye ni muumini na mhudumu wa kanisa Katoliki katika eneo lolote ulimwenguni.
Wakiwa katika eneo la kuchagua Papa mpya, makadinali hawaruhusiwi kuwasiliana na yeyote aliye nje ya eneo hilo na kawaida eneo hilo hukaguliwa vikali kuona kwamba hakuna vifaa vya mawasiliano humo.
Kila kadinali huandika jina la mtu anayempendekeza awe Papa kwenye kijikaratasi na kukitia kwenye chungu fulani. vijikaratasi hivyo hufunguliwa na kuwapa wahusika ufahamu wa wagombea.
Ili kuibuka mshindi ni lazima mgombea atimize thuluthi mbili ya jumla ya kura na ikumbukwe kwamba kadinali aliye na umri wa zaidi ya miaka 80 haruhusiwi kupiga kura.
Shughuli ya kupiga kura hurudiwa hata mara tano kwa siku, hatua ambayo huenda ikaendelea kwa siku kadhaa hadi mmoja wa wagombea atimize kiwango hitajika cha kura.
Mara nyingine makadinali hulazimika kushindanisha wagombea wawili ambayo wamepata kura sawa ili kupata mshindi halisi.
kila mwisho wa siku, vijikaratasi vya kura huchomwa katika eneo fulani maalum ambalo ni la kuwasiliana na walio nje kuhusu unavyoendelea mchakato wa kuchagua Papa.
Kemikali spesheli huongezwa kwenye vjikaratasi hivyo ili kutoa moshi wa rangi nyeusi au nyeupe. Moshi mweusi unaashiria kwamba bado Papa hajachaguliwa huku mweupe ukiashiria kwamba tayari Papa amechaguliwa na hivyo kuhitimisha mchakato huo.
Baadaye papa aliyeteuliwa huonyeshwa kwa waumini wa kanisa katoliki kupitia kwenye roshani ya St. Peters Square na sherehe ya kumtawaza huandaliwa siku chache baadaye.