Waziri wa utumishi wa umma Moses Kuria, ametangaza kuwa serikali imesimamisha uajiri katika utumishi wa umma, hii ikiwa ni njia moja ya kupunguza matumizi serikalini.
Kupitia kwa taarifa siku ya Alhamisi, Kuria alisema hatua hiyo imejiri kufuatia mikakati iliyotangazwa awali na waziri wa fedha Prof. Njuguna Ndung’u, wakati alipowasilisha makadirio ya matumizi ya fedha za serikali bungeni Juni 13, 2024.
“Kwa sasa malipo ya mishahara na marupurupu ni ya viwango vya juu, hali inayohujumu uwezo wetu wa kutenga fedha katika maswala mengine ya kitaifa,” alisema Kuria.
Waziri huyo alisema wakati wa kipindi hicho cha kusitisha uajiri, serikali itafanya ukaguzi wa kina katika orodha ya mishahara ya watumishi wa umma.
Aidha kulingana na Kuria, shughuli za uajiri katika sekta ya umma zitazingatia tu mahitaji maalum ya kipekee.
Kuria alisema hatua hizo zinalenga kuimarisha uchumi wa Kenya, na pia kuhakikisha sekta ya utumishi wa umma unawiana na uwezo wa kifedha wa taifa hili.