Wadau katika sekta ya vyombo vya habari chini ya mwavuli wa Kenya Media Sector Working Group (KMSWG) wameipongeza serikali kwa kuridhia kuondoa Mswada tata wa Fedha 2024.
Hii ni baada ya maandamano yaliyodumu wiki mbili na kuendeshwa na vijana wa Gen Z kuupinga mswada huo.
Wakiongozwa na mwenyekiti wa Chama cha Wahariri nchini (KEG) Zubeida Kananu na mwenyekiti wa Chama cha Wanahabari nchini (KUJ) Erick Oduor, wadau hao wamesema hatua hiyo ya serikali ni ishara tosha kwamba iko tayari kusikiliza na kutatua masuala yaliyoibuliwa kupitia maandaman hayo.
“KMSWG inaipongeza serikali kwa kuondoa Mswada wa Fedha 2024 kufuatia maandamano hayo. Hatua hiyo inaashiria utayari wa kusikiliza na kutatua masuala yaliyoibuliwa,” alisema Kananu wakati wakiwahutubia wanahabari katika hoteli moja jijini Nairobi leo Jumatatu.
“Hata hivyo, masuala msingi bado hayajatatuliwa. Wakenya wakiongozwa na Gen Z wameangazia masuala mbalimbali, kuanzia kwa changamoto za kiuchumi, ukosefu wa ajira kwa vijana na chagamoto za elimu pamoja na haja ya kuwepo kwa uongozi mzuri.”
Huku serikali ikijizatiti kuangazia masuala hayo, KMSWG imesisitiza umuhimu wa vyombo vya habari katika kupatiana jukwaa la masuala hayo kujadiliwa na kutafutiwa ufumbuzi, wajibu ambao inasema kuanzia sasa itatekelezwa kwa kujitolea kwa dhati.
“Tuko tayari kutoa taarifa sahihi, zisizoegemea upande wowote na kutoa ripoti kwa kuwajibika ili kuakisi mitazamo mbalimbali ndani ya jamii ya Kenya.”