Serikali imepiga marufuku uagizaji wa sukari kutoka nchi za nje huku maafisa husika katika viingilio vya nchi wakitakiwa watekeleze marufuku hiyo.
Agizo hilo lilitolewa na katibu katika wizara ya usalama wa taifa Raymond Omollo ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati inayohusika na usimamizi wa mipaka na mipango.
Kulingana na Omollo hatua hiyo inalenga kukuza viwanda vya kutengeneza sukari humu nchini.
Maafisa hao kwenye viingilio vya Kenya pia wamepatiwa ruhusa ya kutekeleza misako ya kutafuta sukari inayoingizwa nchini kimagendo.
Serikali imekuwa ikijitahidi kufufua viwanda vya sukari humu nchini na marufuku ya uagizaji wa sukari kutoka nje ni mojawapo ya njia za kuimarisha ufufuzi huo.
Omollo alisema sukari inayotengenezwa nchini ambayo ni takribani tani elfu 80 kwa wastani kila mwezi inatosha kukidhi mahitaji ya wakenya ambao hutumia takribani tani nne pekee kwa jumla kwa mwezi.
Wenyeviti wa kamati za mpakani katika maeneo ya Namanga, Muhuru Bay, Isebania, Taveta, Moyale, Suam, Oloitoktok, Mbita, Busia, Malaba, Lwakhakha, Mandera na Garissa tayari wamefahamishwa kuhusu marufuku hiyo.
Wahusika katika viwanja vya ndege pia wanafahamu hilo.
Wakulima wa miwa huenda wakapata afueni kutokana na agizo hilo la kusitisha uagizaji wa sukari kutoka nje wakitumai kupata mapato bora kutokana na zao hilo.