Serikali imezuia viwanda vya kusaga unga kuagiza ngano kutoka nje ya nchi, hadi wakulima wa humu nchini watakapomaliza akiba yao ya sasa inayokisiwa kufikia magunia milioni moja
Akiongea alipohudhuria mazishi ya Mzee Titame Ole Sankei eneo la Narok Magharibi, kaunti ya Narok, Rais William Ruto alisema viwanda hivyo vitaruhusiwa kuagiza ngano baada ya kununua kutoka kwa wakulima wa humu nchini.
Kiongozi wa nchi alisema kampuni hizo zinapaswa kwanza kumaliza kinachopatikana humu nchini kabla ya kuagiza kutoka nje.
Kuhusu bei ya mahindi, rais Ruto aliwaahidi wakulima kwamba serikali itatangaza bei nzuri ya mahindi yao.
Aidha Rais Ruto aliwahimiza viongozi na wakazi wa jamii ya wamaasai kuunga mkono miradi ya serikali ya kitaifa katika eneo hilo, akisisitiza kwamba atajaribu kulinda chemi chemi za maji kama vile msitu wa Mau dhidi ya kunyemelewa.