Serikali imemtetea balozi wa Marekani humu nchini Meg Whitman kufuatia matamshi yake aliyotoa kuhusiana na uchaguzi mkuu wa mwaka uliopita.
Huku akimtetea balozi huyo, Rais William Ruto aliwataka wanasiasa kukoma kuhujumu uhusiano wa kimataifa wa taifa hili.
Rais Ruto alimkosoa kiongozi wa upinzani Raila Odinga kwa kumshambulia balozi wa Marekani nchini Kenya Meg Whitman, akisema hatua hiyo inadhoofisha uhusiano kati ya Kenya na Marekani.
Aliyataja maoni ya Raila kuwa ya kizembe, ya kibinafsi na yasiyostahili.
Rais Ruto alisisitiza kwamba matamshi ya Whitman kuhusu uchaguzi wa mwaka jana yalikuwa ya kweli na sahihi.
Alisema ni jambo la kusikitisha kwamba Raila aliona inafaa kuenzi ghasia na uharibifu wa mali bila kujali maslahi ya nchi duniani.
“Tutakuwa wasio na shukrani sana kuwakashifu watu ambao wanatutengenezea fursa,” alisema Ruto.
Akiongeza kuwa, “Kati ya watu wanaopanga uharibifu wa mali na kuhujumu uchumi wetu na wale wanaofanya kazi nasi kubuni fursa za uwekezaji, nani mhuni?
Rais Ruto alisema Marekani ni mojawapo ya washirika wa karibu wa kibiashara na uwekezaji wa Kenya, unaosimamia zaidi ya shilingi bilioni 200 kwa mwaka.
Aliongeza kuwa uwekezaji huo ni muhimu kwa ukuaji na maendeleo ya nchi.
“Lazima tujue maslahi yetu ni nini, na lazima tulinde maslahi hayo.”