Serikali yalaani matamshi ya Naibu Rais wa zamani Rigathi Gachagua kuhusu pombe haramu

Katika taarifa Idaraya usalama wa ndani na utawala wa kitaifa, inatilia shaka uzito wa tuhuma hizo, hasa kutokana na juhudi za kitaifa zinazoendelea za kupambana na tatizo la matumizi mabaya ya dawa za kulevya.

Marion Bosire
4 Min Read

Idara ya Usalama wa Ndani na Utawala wa Kitaifa imekemea vikali kauli za hivi karibuni za aliyekuwa naubu rais Rigathi Gachagua, ambaye, wakati wa ibada ya Jumapili, alidai kwamba serikali inalenga raia wa eneo la Mlima Kenya kwa kusambaza pombe haramu.

Katika taarifa iliyotolewa leo, Idara hiyo inatilia shaka uzito wa tuhuma hizo hasa kutokana na juhudi za kitaifa zinazoendelea za kupambana na tatizo la matumizi mabaya ya dawa za kulevya.

Taaarifa hiyo ilisisitiza madhara makubwa ya pombe haramu kwa watu na familia, ikitaja vifo vya kusikitisha vya wakenya watatu huko Nakuru wikendi iliyopita kutokana na sumu ya pombe.

Serikali inasisitiza kujitolea kwake kukabiliana na matumizi mabaya ya pombe na madhara makubwa inayosababisha kwa afya ya umma na maisha ya familia.

“Tunashutumu vikali dharau kwa suala hili muhimu la kitaifa,” alisema Dkt. Raymond Omollo, Katibu wa Idara ya Usalama wa Ndani na Utawala wa Kitaifa.

“Kutoa tuhuma za aina hii, hasa katika jukwaa la kanisa, bila huruma kwa wanaolia na kupambana na madhara ya pombe haramu ni kitendo kisichofaa.” aliendelea kusema Omollo.

Idara hiyo ilifafanua zaidi kwamba serikali haitengenezi wala kusambaza pombe na inapuuzilia mbali matamshi ya Gachagua kama ya kisiasa na yakupotosha.

Aidha, ilieleza kwamba maafisa wa serikali, wakiwemo machifu na wasaidizi wao, wanashiriki kikamilifu vita dhidi ya pombe haramu, wakifanya kazi katika jamii zao kushughulikia suala hili.

Idara hiyo inakatalia mbali pendekezo kwamba kuna mfanyakazi yeyote wa serikali anahusika na uuzaji wa pombe hatari au bandia.

Juhudi za serikali za kupunguza tatizo la pombe haramu zipo wazi.

Mwe Machi 2024, ilianzisha mpango wa utekelezaji wa hatua 25 ukilenga utengenezaji, uuzaji na usambazaji wa pombe haramu na dawa nyingine hatari.

Kama sehemu ya mpango huu, wazalishaji 29 wa pombe ya kiwango cha pili walikaguliwa na kundi la maafisa wa mashirika mengi, ambapo wawili tu walipatikana kutii sheria kikamilifu.

Zoezi la pili lilifanyika kwa wafanyabiashara walioshindwa awali, ambapo watengenezaji pombe 13 pekee walipatiwa leseni.

“Hili ni suala zito linalohusiana na afya na usalama wa Wakenya na kutoa tuhuma zisizo na msingi bila ushahidi ni kuharibu juhudi zinazoendelea za kulinda raia,” alisema Dkt. Omollo.

Aliongeza kusema kwamba iwapo Gachagua ana ushahidi wa kudhibitisha madai yake, auwasilishe kwa mamlaka husika za uchunguzi ili hatua stahiki zichukuliwe.”

Serikali inatoa wito kwa Wakenya wote kushirikiana ili kulinda jamii zao msimu huu wa sherehe na kulinda watoto kutokana na hatari ya matumizi ya dawa za kulevya.

Hatua kuu zilizotajwa katika taarifa hiyo ni pamoja na kuhamasisha jamii, kuwajibisha jamii, kuzuia ulevi na kuendesha magari na kupunguza upatikanaji wa pombe nyumbani kwa watoto wadogo.

Umma pia unahimizwa kuripoti uuzaji wa pombe haramu.

“Sote lazima tutekeleze majukumu yetu katika kushughulikia janga hili, si tu kupitia hatua za serikali, bali kupitia jukumu letu la pamoja katika nyumba zetu, shule zetu na jamii zetu” alimaliza Dkt. Omollo.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *