Serikali yakabiliana na vifo vya watoto wanaozaliwa kabla ya muda wao kutimia

Tom Mathinji
1 Min Read

Waziri wa afya Susan Nakhumicha amesisitiza umuhimu wa kushughulikia visa vya kufariki kwa watoto wachanga hasa wale wanaozaliwa kabla ya muda wao kutimia.

Waziri huyo amesema Kenya inanuia kupunguza kiwango cha sasa cha vifo vya watoto wachanga ambapo watoto 21 kati ya 1,000 wanaozaliwa hadi 12 mwaka wa 2030, kuambatana na malengo ya maendeleo endelevu.

Waziri Nakhumicha alisema mipango kama vile Kangaroo Mother Care-KMC na juhudi za kutoa mafunzo kwa wahudumu wa afya ni muhimu katika kuafikia malengo hayo.

Kwenye hotuba iliosomwa kwa niaba yake na kaimu mkurugenzi wa afya Dkt. Patrick Amoth, wakati wa siku ya kukomesha vifo vya watoto kabla ya muda wao wa kuzaliwa kutimia, iliyohudhuriwa na gavana wa Makueni Mutula Kalonzo, waziri huyo alielezea athari zinazowakabili watoto wanaozaliwa kabla ya muda wao.

Alisema mnamo mwaka wa 2020, watoto 127,500 walizaliwa kabla ya muda wao kutimia ambayo ni sawa na asilimia 12.

Mataifa ya kusini mwa jangwa la Sahara yanaongoza kwa idadi ya watoto wanaofariki ikiwa ni watoto 27 kwa kila 1,000 wanaozaliwa, sawa na asilimia 43 ya idadi ya jumla ya watoto wanaozaliwa kabla ya muda wao kutimia duniani.

Share This Article