Katibu wa baraza la mawaziri Mercy Wanjau, ametoa wito kwa taasisi za serikali ambazo bado zinatumia nambari tofauti za paybill isipokuwa ile ya 222222, kuzifunga kufikia tarehe 15 mwezi ujao.
Akizungumza alipokutana na makatibu na wakuu wa taasisi 17 za serikali zinazoleta kiwango cha juu cha mapato ambazo bado hazijatimiza agizo la serikali la kuhamia mfumo wa kidijitali wa e-citizen, Wanjau alisema mashirika ya serikali yanaendelea kuhamia mfumo huo huku ukusanyaji mapato ukiongezeka.
Kulingana na katibu huyo, kufikia sasa wizara, idara na mashirika 250 yamehamia kikamilifu mfumo wa e-Citizen, ambapo yanatoa huduma elfu-16 za serikali kutoka huduma 397 mwezi Juni mwaka uliopita na kukusanya mapato ya shilingi milioni 281 kwa siku.
Alisema kuwa mashirika yote ya serikali yakihamia mfumo huo mapato ya kila siku yatapita zaidi ya shilingi bilioni moja kwa siku.
Kwa upande wake, katibu katika idara ya uhamiaji na huduma kwa wananchi Julius Bitok, alisema wanalenga kuunganisha idara tofauti na kwamba huduma zao zitapatikana hivi karibuni.
Akizindua huduma za serikali kwenye mfumo wa E-Citizen tarehe 30 mwezi Juni mwaka huu, Rais William Ruto aliagiza kwamba mashirika yote ya serikali yahamishie huduma zao mtandaoni.
Uhamiaji huo unanuiwa kuimarisha utoaji huduma na wakati huo huo kuziba mianya katika ukusanyaji ushuru.