Naibu Rais Kithure Kindiki, amesema kwamba serikali imejitolea kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora na sawa za afya kwa wote.
Akizungumza alipozuru hospitali ya rufaa ya kitaifa ya Kenyatta jijini Nairobi, Kindiki alisema kwamba serikali inafuatilia kwa makini ili kuhakikisha wagonjwa wanaotumwa kutoka hospitali za kiwango cha chini wanashughulikiwa ipasavyo.
Kindiki aliyekuwa akitekeleza utathmini wa utekelezaji wa mpango wa Taifa Care, alisema serikali inajizatiti pia kuongeza uwezo wa hospitali za kiwango cha chini wa kutambua magonjwa.
Kulingana naye hatua hiyo itaimarisha ufaafu wa rufaa ili kupunguza athari za magonjwa hasa kwa wakenya wa kipato cha chini ambao hawajakuwa wakipata huduma za afya.
Alisema hilo litaafikiwa kupitia kwa wakenya wengi kujisajili kwa halmashauri ya afya ya jamii nchini SHA, ili wapate huduma chini ya mpango wa Taifa Care.
Kindiki alipongeza pia chuo kikuu cha Nairobi na taasisi ya masomo ya sayansi ya afya kwa kutoa usaidizi unaohitajika na wahudumu wa afya kwa hospitali ya kitaifa ya Kenyatta.
Alisema kwamba afya inagusa sekta kadhaa na ili utoaji wa huduma za afya ufanikiwe, lazima kuwe na wahudumu waliohitimu.
Kiongozi huyo aliongeza kusema kwamba kukamilishwa kwa taasisi ya figo ya Afrika mashariki katika shule ya masomo ya sayansi ya afya kutasaidia pia hospitali ya Kenyatta.
Anahisi kwamba kitengo cha matibabu ya magonjwa ya figo kitaimarika zaidi kufuatia ujio wa taasisi hiyo ya masomo ya figo.