Waziri wa usalama wa taifa Kithure Kindiki amesema serikali inaimarisha uwezo wa shirika la kupambana na matumizi ya dawa za kulevya NACADA ili kukabiliana na upatikanaji wa pombe haramu, mihadarati na dawa nyingine za kulevya kama njia ya kupiga jeki mpango unaoendelea wa kitaifa wa kumaliza matumizi mabaya ya dawa za kulevya na pombe.
Kindiki alisema biashara na matumizi ya dawa hizo za kulevya ni moja kati ya vitisho vitano vikuu vya usalama wa taifa ambavyo vinajumuisha ugaidi, ujambazi na wizi wa mifugo, itikadi kali za kitamaduni kidini na kisiasa na mabadiliko ya tabianchi.
“Tunapongeza ushirikiano wa serikali kuu na serikali za kaunti katika kutokomeza zimwi la matumizi ya pombe haramu na dawa za kulevya.” alisema waziri Kindiki akiongeza kwamba ushirikiano huo unahusisha ujenzi wa vituo vya matibabu na kurekebisha tabia watumizi wa mihadarati na pombe.
Alielezea kwamba shirika la NACADA limeanzisha mpango wa kufuatilia watu ambao wamepitia vituo kama hivyo ili kuwasaidia kupata ujuzi na kuanzisha mipango ya kujipatia riziki.
Kulingana naye hiyo ni njia moja ya kuweka huru vijana wengi ambao walidanganywa na wanabiashara wa biashara hiyo haramu na kuishia kuwa waraibu wa dawa hizo na pombe.
Waziri Kindiki alisema haya alipozuru na kuidhinisha kituo cha matibabu na kurekebisha tabia cha Ihururu ambacho kiko katika eneo bunge la Tetu kaunti ya Nyeri.
Alikuwa ameandamana na naibu gavana wa kaunti ya Nyeri David Kinaniri, wakurugenzi na wasimamizi wa shirika la NACADA pamoja na wakazi wa wadi ya Dedan Kimathi.