Serikali inahitaji shilingi milioni 400 kuwezesha mchakato wa kuwarejesha nyumbani Wakenya zaidi ya laki 5 waliokwama katika nchi mbalimbali za eneo la Mashariki ya Kati linalokumbwa na vita.
Haya yalibainika kwenye kikao cha kamati ya Bunge la Taifa kuhusu ulinzi, ujasusi na mahusiano ya kimataifa na maafisa wa idara ya masuala ya ughaibuni leo Alhamisi.
Wakiongozwa na Balozi Hellen Gichuhi ambaye ni Katibu wa Maslahi ya Wakenya walio ughaibuni na ushirikiano, maafisa hao walisema kufikia sasa ni Wakenya 15 pekee wameokolewa kutoka Mashariki ya Kati.
Wakenya hao 15 wanaojumuisha watoto watano, wanaripotiwa kusafiri kwa njia ya gari kutoka Mashariki ya Kati hadi Uturuki na wanatarajiwa kuabiri ndege leo kurejea nyumbani.
Balozi Gichuhi aliambia wabunge kwamba mchakato wa urejeshaji wa Wakenya hao nyumbani utatekelezwa kwa njia ya kipaumbele ambapo watoto na wakongwe wataangaziwa kwanza.
Kulingana naye, kuna baadhi ya Wakenya ambao hawajawasiliana na balozi za Kenya katika mataifa waliyomo na huenda wameamua kusubiri hadi vita vinavyoendelea vimalizike na waendelee na kazi.
Marekani kwa ushirikiano na Israel ilivamia Iran siku ya mwisho ya mwezi Februari mwaka huu, hatua ambayo ilisababisha mashambulizi ya kulipiza kisasi ambayo yameathiri nchi kadhaa za Mashariki ya Kati.