Serikali yafafanua kuhusu sheria za Visa za kazi kwa wageni

Waziri Lee Kinyanjui ameonya kuwa wageni wanaojihusisha na shughuli zilizo nje ya masharti ya hadhi yao ya uhamiaji wanaweza kupokonywa visa.

Marion Bosire
2 Min Read
Lee Kinyanjui, Waziri wa Uwekezaji, Biashara na Viwanda.

Serikali ya Kenya imefafanua kuwa mfumo wake wa kuingia nchini bila visa hauwapi wageni haki ya moja kwa moja ya kufanya kazi, biashara au kuendesha shughuli za kibiashara humu nchini.

Waziri wa Uwekezaji, Biashara na Viwanda, Lee Kinyanjui, alitoa ufafanuzi huo jana Septemba 6, akionya kuwa wageni wanaojihusisha na shughuli zilizo nje ya masharti ya hadhi yao ya uhamiaji wanaweza kupokonywa visa zao.

Taarifa hiyo inafuatia wasiwasi kuhusu wageni wanaoingia Kenya kama watalii au wawekezaji, kisha kujihusisha na biashara za rejareja na biashara za ndani bila vibali vya kazi na idhini zinazohitajika.

Kinyanjui alisisitiza kuwa kuingia nchini bila visa na msamaha wa mahitaji ya mfumo wa uidhinishaji wa kielektroniki wa usafiri, ETA, kunarahisisha tu kuingia nchini na hakuchukui nafasi ya mahitaji ya uhamiaji, vibali vya kazi au masharti mengine ya kisheria.

Maafisa wa serikali walisema baadhi ya wageni wamekuwa wakitumia vibaya hadhi ya utalii au uwekezaji, hali iliyosababisha haja ya kuhakikisha shughuli zao zinaendana na masharti ya vibali na hati walizopatiwa.

Wageni watakaobainika kukiuka masharti ya visa wanaweza kufutiwa visa zao kwa mujibu wa sheria.

Kenya ilianzisha mfumo wa kuingia bila visa kwa wageni kutoka duniani kote Januari 2024, na baadaye ikaondoa mahitaji ya ETA kwa raia wa nchi nyingi za Afrika Januari 2025.

Serikali imesema hatua hizo zimekuza utalii na uwekezaji na zitaendelea, huku utekelezaji ukifanyika kwa utaratibu na uwazi. Imesema pia kwamba utekelezaji huo utazingatia kikamilifu ahadi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC.

Mamlaka zimesisitiza kuwa sera hiyo hailengi kuwakatisha tamaa wawekezaji halali wa kigeni. Badala yake, wageni wanaotaka kufanya kazi, biashara au kuendesha shughuli za kibiashara lazima wapate vibali vinavyofaa na kuzingatia sheria za Kenya.

Share This Article