Wafanyabiashara wadogo wadogo wana sababu ya kutabasamu baada ya serikali kuamuru kuachiliwa kwa bidhaa zao zinazozuiliwa katika bandari ya Mombasa.
Agizo hilo lilitolewa na Naibu Rais Rigathi Gachagua siku ya Alhamisi.
Hata hivyo, alisema bidhaa hizo kwanza zitakaguliwa katika muda wa majuma mawili yajayo ili kuhakikisha bidhaa ghushi haziingii hapa nchini.
Katika mkutano na wafanyabiashara wadogo wadogo katika makazi yake mtaani Karen, Gachagua alisema serikali pia imebatilisha uamuzi wa nyongeza ya ushuru wa forodha kutoka shilingi milioni 2.5 hadi milioni 3 kwa kila shehena.
Wafanyabiashara hao walikuwa wamelalamikia ada ya ziada ya shilngi nusu milioni waliyotozwa huku wakiitaja kama isiyofaa.
Naibu Rais alisema wafanyabiashara hao watakabidhiwa cheti kimoja kilichowianishwa kutoka mamlaka ya kupambana na bidhaa ghushi na shirika la kukadiria ubora wa bidhaa, badala ya ukaguzi wa bidhaa na mashirika hayo mawili ya serikali.
Wakati huo huo, aliamuru mamlaka ya kupambana na bidhaa bandia kuwachukulia hatua maafisa wanaotuhumiwa kusumbua wafanyabiashara wakati wa ukaguzi wakisingizia kutafuta bidhaa bandia.