Serikali ya taifa jirani la Uganda imetoa tahadhari kwa umma kuhusu mvua inayotizamiwa ya Elnino.
Katika taarifa kutoka kwa afisi ya waziri mkuu ambayo imetiwa saini na katibu wa kudumu Irumba Rogers Kaija, kamati za kusimamia majanga katika kiwango cha wilaya wamepatiwa maelekezo.
Kulingana na ripoti ya mamlaka ya utabiri wa hali ya hewa nchini humo ya mwezi Septemba hadi Disemba, mvua kubwa inatarajiwa katika kipindi hicho nchini Uganda.
Inatarajiwa kwamba maisha ya wakazi wa nchi hiyo huenda yakaathirika kwa sababu mvua ya El Nino inahusishwa na mabadiliko makubwa katika hali ya hewa.
Wasimamizi wa majanga katika kila wilaya wametakiwa waimarishe mipango ya kukabiliana na majanga, waelimishe umma kuhusu hatari za mvua hiyo, wawe wakitekeleza ukaguzi wa kila mara nyanjani, wapokee ripoti za utabiri wa hali ya hewa na kuzitathmini kati ya hatua nyingine.
Wananchi nao wameelekezwa watekeleze usafi katika maeneo yao ikiwa ni pamoja na kuondoa takataka na kuzibua mitaro ya kupitisha maji.
Wamehimizwa pia wajiwekee akiba ya chakula, wanaoishi kwenye maeneo hatari wahame, wasivuke mito iliyofurika, waandae vifaa vya kuteka na kuhifadhi maji ya mvua, wasitumie usafiri wa majini na wasijikinge mvua chini ya miti.
Hali ya El Nino inajiri katika bahari ya Pacific na inaaminika kwamba itasababisha kiwango cha juu cha mvua katika maeneo kadhaa kati ya Septemba na Disemba 2023.