Serikali ya kaunti ya Nairobi kuwahamisha waathiriwa wa mafuriko

Tom Mathinji
1 Min Read
Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja.

Gavana wa kaunti ya Nairobi Johnson Sakaja, ameagiza kuhamishwa kwa zaidi ya wakazi 3,000 wa jiji hilo ambao wameathiriwa na mafuriko, kufuatia mvua kubwa inayoshuhudiwa hapa nchini.

Akizungumza baada ya kuzuru maeneo ambayo yameathirika pakubwa na mafuriko hayo, Gavana huyo alisema takriban watu 60,000, haswa wanawake na watoto wameathiriwa pakubwa na mafuriko hayo.

“Licha ya kwamba tunakabiliwa na janga la kibinadamu, operesheni kubwa inatekelezwa chini ya uongozi wangu. Tunatarajia kuwahamisha watu 3,000 hadi katika makazi ya muda,” alisema Gavana Sakaja.

Kulingana na Gavana huyo, watu wanne wamethibitishwa kufariki kutokana na mafuriko hayo, huku wengine sita wakiwa hawajulikani waliko.

Maeneo yaliyoathirika pakubwa na mafuriko hayo ni pamoja na  Kibra, Lindi, Mathare 4A, Mathare North, Baba Dogo, Githurai na Zimmerman.

Aidha Gavana huyo alizitaka kampuni za kibinafsi za kuzoa taka, kuhakikisha taka zote zinapelekwa katika kituo cha utupaji taka kilicho katika mtaa wa Dandora, huku akionya kuwa zile zitakazokiuka agizo hilo zitachukuliwa hatua.

Sakaja amewaagiza wanaoishi karibu na mito kuondoka mara moja.

Share This Article