Jamaa za raia wa Israel ambao walishikwa mateka na wapiganaji wa Hamas huko Gaza wameitaka serikali ya nchi yao kukubali mpango wa Rais Joe Biden wa Marekani wa kusitisha mapigano.
Katika kikao chao na wanahabari Jumamosi, wanachama wa kundi la watu ambao jamaa zao walipotea au kushikwa mateka na Hamas walisema kwamba wanataka raia wa Israel wafanye maandamano ili kuhakikisha mpango huo unatekelezwa kikamilifu.
Watu hao wanaamini kwamba waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anakwaza mpango huo baada ya Biden kutangaza Ijumaa kwamba Israel imetoa mapendekezo mapya ya kusitisha mapigano.
Mpango wa awamu tatu uliopendekezwa na Biden unalenga kuhakikisha vita vinasitishwa kabisa katika ukanda wa Gaza na unahusisha kuondolewa kabisa kwa wanajeshi wa Israel katika sehemu zenye watu wengi za ukanda huo.
Kundi la Hamas lilionekana kukubali mpango huo wa Marekani likisema lingependa vita visitishwe kabisa Gaza, wanajeshi waondolewe huko kabisa, eneo hilo lijengwe upya, watu warejeshwe makwao na wabadilishane mateka.
Lakini Netanyahu jana alikana mpango huo akisema vita vitasitishwa wakati kundi la Hamas litamalizwa kabisa na mateka wote wa mapigano hayo ya miezi minane kuachiliwa.
Familia za mateka wa mapigano hayo zinahisi kwamba Netanyahu anashinikizwa kushikilia msimamo mkali na watu fulani kwenye serikali ya Israel.
Shirika la habari la Axios la Marekani lilisema kupitia mtandao wa X kwamba mawaziri wa Israel Itamar Ben-Gvirna Bezalel Smotrich wametishia kuondoka kwenye muungano wa kisiasa unaotawala na kupindua serikali iwapo mpango wa Biden wa kusitisha vita utatekelezwa.
Watu wapatao elfu 36 wamefariki kwenye mashambulizi ya Israel katika ukanda wa Gaza, wengine zaidi ya elfu 82 wamejeruhiwa na wengine wengi wamepoteza makazi yao.
Israel ilianzisha mashambulizi hayo kama njia ya kulipiza kisasi mashambulizi ya kundi la Hamas ya Oktoba 7, 2023 katika sehemu mbali mbali za Israel.