Serikali ya nchi ya Congo Brazzaville imekanusha madai ya jaribio la mapinduzi ya serikali nchini humo.
Hii ni baada ya uvumi kuenea mitandaoni kwamba wanajeshi walijaribu kupindua serikali ya Rais Denis Nguesso ambaye yuko nchini Marekani kwa sasa kwa ajili ya kikao cha Umoja wa Mataifa.
Nguesso wa umri wa miaka 79 amekuwa madarakani kwa muda wa miaka 39.
Waziri wa mawasiliano nchini Congo Brazzaville Thierry Moungalla alitumia mtandao wa X ambao awali ulifahamika kama Twitter kukanusha madai hayo.
Alihakikishia umma kwamba nchi ni tulivu na waendeleze shughuli zao za kawaida.
Haya yanafuatia misururu ya mapinduzi ya serikali za nchi kadhaa Barani Afrika.
Mapinduzi ya hivi karibuni zaidi yalitokea nchini Gabon punde baada ya uchaguzi mkuu ambapo Rais Ali Bongo Ondimba alitangazwa mshindi.
Ali alikuwa ameongoza nchi hiyo tangu mwaka 2009 wakati babake Rais Omar Bongo aliaga dunia.