Serikali na KMPDU zaongezewa siku mbili kumaliza mgomo wa madaktari

Tom Mathinji
1 Min Read
Madaktari washiriki mgomo kushinikiza kuajiriwa kwa Madaktari wanagenzi.

Mahakama ya kushughulikia mizozo ya wafanyakazi, imekipa chama cha madaktari na wataalamu wa meno nchini (KMPDU) na serikali muda wa siku mbili zaidi kuafikia mkataba wa pande mbili wa kurejea kazini wenye usawa.

Jaji Byram Ongaya wa mahakama kuu, alisema muda huo umeongezwa ili kuimarisha mashauriano na kuepusha suluhu ya upande mmoja.

Jaji Ongaya aliziagiza pande hizo mbili zihitimishe mashauriano yao na kutia saini mkataba wa kurejea kazini kabla ya kesi hiyo kusikizwa May, 8, 2024,  saa nane unusu alasriri.

Jaji Ongaya alisema anawapa fursa ya mwisho akionya pande hizo mbili kwamba mahakama hiyo itatoa uamuzi wake kuhusiana na mgomo huo unaoendelea ambao umekwamisha huduma za matibabu katika hospitali za umma kote nchini kwa zaidi ya siku 50.

Juma lililopita mahakama kuu ilikuwa imeiagiza serikali na madaktari wanaogoma kutia saini mfumo wa kureja kazini utakaoidhinishwa na mahakama leo Jumanne.

Jaji Ongaya alikuwa ameziagiza pande hizo mbili ziweke kando swala la mishahara ya madaktari wanagezni akisema kesi hiyo tayari iko kwenye mahakama ya Eldoret.

Chama hicho cha madaktari kimesema kuwa kiko tayari kwa mashauriano na serikali kiksiema kuwa mkataba wa nyongeza ya mishahara na makubaliano mengine ni sharti yatekelezwe ili warejee kazini.

TAGGED:
Share This Article